MIMINA MOYO WAKO KWA MUNGU

David Wilkerson (1931-2011)

Mara nyingi watu wanatuandikia wakisema, “Sina mtu wa kuzungumza naye, hakuna wa kushiriki naye mzigo wangu. Hakuna mtu ana wakati wa kusikia kilio changu. Nahitaji mtu ninayeweza kumwaga moyo wangu kwake.”

Mfalme Daudi alizungukwa na watu. Alikuwa ameoa akiwa na familia kubwa na alikuwa na waandamani wengi kando yake, lakini tunasikia kilio kile kile cha Daudi: “Nitaenda kwa nani?” Ni katika asili yetu kutaka binadamu mwingine awepo, atusikilize na atushauri.

Ayubu alipolemewa na majaribu yake, alilia kwa huzuni, “Laiti ningalikuwa na mtu wa kunisikia!” (Ayubu 31:35). Alitoa kilio hiki akiwa ameketi mbele ya wale waliojiita marafiki zake ambao hawakuwa na huruma kwa matatizo ya Ayubu. Badala yake walikuwa ni wajumbe wa kukata tamaa.

Katika huzuni yake, Ayubu alimgeukia Bwana. “Hakika hata sasa shahidi wangu yuko mbinguni, na ushahidi wangu uko juu. Rafiki zangu hunidharau; macho yangu yamwagilia Mungu machozi” (Ayubu 16:19-20).

Katika Zaburi, Daudi aliwahimiza watu wa Mungu wafanye vivyo hivyo. “Mtumainini yeye nyakati zote; mimina moyo wako mbele zake; Mungu ni kimbilio letu. Sela” (Zaburi 62:8) na “Namlilia Bwana kwa sauti yangu; kwa sauti yangu namwomba Bwana dua yangu. Namimina malalamiko yangu mbele zake; Ninatangaza mbele zake shida yangu. Roho yangu ilipozimia ndani yangu, ndipo ulipoijua njia yangu. Katika njia ninayotembea…. Nilikulilia, Ee Bwana, nalisema, Wewe ndiwe kimbilio langu, sehemu yangu katika nchi ya walio hai” (Zaburi 142:1-5).

Ninaamini moyoni mwangu kwamba ujumbe huu ni mwaliko kwako kutoka kwa Roho Mtakatifu kupata mahali pa faragha ambapo unaweza kumimina nafsi yako kwa Bwana mara kwa mara. Unaweza kuzungumza na Yesu kuhusu kila kitu—shida zako, majaribu yako ya sasa, fedha, afya—na kumwambia jinsi ulivyolemewa, hata jinsi umevunjika moyo. Atakusikia kwa upendo na huruma, na hatadharau kilio chako. Kwa karne nyingi amejibu kilio cha moyo cha kila mtu ambaye ameamini ahadi zake. Kadhalika ameahidi kukusikia na kukuongoza. Hakika amekuahidi kwa kiapo kuwa ni nguvu yako. Nenda kwake, nawe utatoka ukiwa wapya.